top of page

Mwandishi:

Mhhariri

ULY CLINIC

Dkt. Benjamin L, MD

Alhamisi, 21 Novemba 2024

Shinikizo la chini la damu

Shinikizo la chini la damu

Kushuka kwa shinikizo la damu ama Shinikizo la chini la damu huweza kuonekana ni hali nzuri kwa baadhi ya watu, lakini ukweli ni kwamba kwa watu wengi hupelekea wapate kizunguzungu na kuzimia. Kama shinikizo ndani ya mishipa ya damu ikishuka kwa kiwango kikubwa mtu anaweza kupoteza maisha.


Ili isemekane kuwa shinikizo ndani ya mishipa ya damu ya mtu limeshuka kupita kiasi huwa hivi, Shinikizo la sistoliki huwa chini ya 90 na shinikizo la dayastoliki kuwa chini ya 60. Kwa kawaida shinikizo la damu hurekodiwa kama namba mbili ya juu na ya chini, namba ya juu huwa shinikizo la sistoliki na ya chini ni la dayastoliki.


Kuna visababishi kadhaa vya shinikizo la chini la damu kama vile kuishiwa maji mwilini, au magonjwa., ni muhimu kujua kisababishi ili kupata matibabu sahihi.

 

Dalili

​Endapo dalili zifuatazo zitatokea, humaanisha kuna tatizo la kupewa kipaumbele kwenye uchunguzi na tiba;

​

Madhara ya shinikizo la chini la damu

Shinikizo la chini la damu kupita kiasi huweza kusababisha mshituko wa moyo. Hali hii huweza kusababisha mtu kupoteza maisha endapo hatapata matibabu ya haraka.

​

Dalili za mtu mwenye mshituko wa moyo ni

  • Kuchanganyikiwa, hasa kwa watu wazima

  • Kuhisi baridi, ngozi kupauka rangi yake (kuwa nyeupe)

  • Kupumua haraka haraka ama kuhemea juu juu

  • Midundo ya mapigo ya mishipa ya damu kuongezeka na kutokuwa na nguvu

​

Endapo unapata dalili zinazoashiria kuwa una mshituko wa moyo inakupasa kuonana na daktari haraka. Endapo pia shinikizo lako la dmau hushuka mara kwa mara, inakupasa kuonana na daktari.

 

Visababishi

Shinikizo la damu ni kipimo cha kasi ya mzunguko wa damu katika mishipa ya ateri unaotokana na msukumu wa damu kwenye Moyo. Shinikizo la damu limegawanyika kwenye sehemu mbili, shinikizo la sistolikic na shinikizo la dayastoliki

 

Shinikizo la sistoliki hutokea pale moyo unapokuwa unadunda, na lile la dayastoliki hutokea moyo unapomaliza kudunda. Visababishi vya kupanda kwa shinikizo la damu huweza kuwa pamoja na sababu zinazoweza kusababisha kuongezeka kwa shinikizo la juu au la chini la damu. Kwa sasa inafahamika kuwa shinikizo la damu la kawaida halitakiwi kuwa chini ya 120/80mmHg.

 

Shinikizo la damu hubadilika mara nyingi kwa siku, ikitegemea shughuli anazofanya mtu kama amekaa na kutembea, akipata mshituko au akiwa na furaha au akiwa anakula au kunywa dawa aina fulani. Hata hivyo shinikizo la damu huwa la chini wakati wa usiku mtu akiwa amelala na hupanda zaidi mtu akisimama au kuamka ghafla.


Mtu anaposimama au kuamka ghafla kutoka kwenye pozi la kulala, husabaisha shinikizo la damu kushuka hivyo kupatwa na dalili ya kizunguzungu au kuzimia, hii ni kwa sababu ubongo wako unakosa damu ukisimama ghafla.

 

Hali zinazosababisha kushuka kwa shinikizo la damu

​

Ujauzito

​

Mishipa ya damu hutanuka wakati wa ujauzito hivyo kupelekea kushuka kwa shinikizo la damu. Hii ni sawa na maji yapotembea katika bomba kubwa yatakuwa na kasi ndogo, vilevile kiasi cha maji yale yale yakipitishwa kwenye bomba lenye kipenyo kidogo (jembamba) yatakuwa na msukumo mkubwa na kuruka mbali. Hali hii ni sawa na damu inayotembea kwenye mishipa. Ujauzito unapoisha shinikizo la damu hujirudia kwenye hali yake ya kawaida.

​

Matatizo ya moyo

​

Matatizo ya moyo yanayoweza kusababisha tatizo la kushuka kwa shinikizo la damu ni pamoja na moyo kudunda taratibu sana, magonjwa ya milango ya moyo, mshituko wa moyo na kufeli kwa moyo

 

Matatizo ya kihomoni

​

Magonjwa ya tezi shingo mfano, ugonjwa wa parathairoid, upungufu wa homoni ya tezi ya adreno, upungufu wa sukari mwilini na ugonjwa wa kisukari huweza kuleta shinikizo la chini la damu.

​

Kuishiwa maji mwilini

​

Matatizo yoyote yanayopelekea kuishiwa maji mwilini husababisha shinikizo la chini la damu. Mfano ni pipa likiwa na maji mengi ukaweka mpira ili kuyatoa, mwanzoni yatatoka kwa kasi na kuruka mbali lakini yakifika mwisho yatapunguza kazi na kuruka karibu, hii ni sawa na shinikizo la damu, endapo maji kwenye damu yamepungua basi mtu huyu hupata shinikizo la chini. Magonjwa na hali zinazoweza kusababisha shinikizo la chini huwa pamoja na, homa, kutapika, kuharisha sana, kutumia dawa za kupunguza maji (kuongeza kukojoa)  na kufanya mazoezi makali.

​

Kutokwa na damu

​Kutokwa na damu kunaweza sababishwa na kujikata, kutokwa damu haimaanishai ni lazima uione damu inamwagika kwa nje, baadhi ya sababu hupelekea kuvilia kwa damu ndani ya mwili, mfano kupasuka kwa ini, bandama au mimba ilitotungiwa nje ya kizazi. Hata hivyo huambatana na dalili zingine za tumbo kuuma. Kutokwa na damu nyingi kutokana na kujikata au kupata ajali husababisha kupoteza maji na chembe za damu. Matokeo yake ni kushuka kwa shinikizo la damu.

​

Homa ya damu

​

Homa ya damu au septisemia hutokana na maambukizi ya virusi, bakteria au fangasi kwenye damu ambapo husababishwa mwitikio wa mishipa ya damu kwa kuongeza chembe za michomo kinga zinazopelekea kuongezeka kwa kipenyo cha mishipa ya damu na hivyo kushusha shinikizo al damu.

​

Mzio mkali

​Mizio au aleji hweza sababishwa na mambo mbalimbali mfano poleni za maua, vumbi, au kula chakula aina fulani. Pia baadhi ya dawa zinaweza kusababisha mzio kwa mtu zikiwepo kama antibayotiki jamii ya penicillin, sumu ya wadudu warukao na nyoka. Mtu akipata mzio mkali huweza kupata dalili za kushindwa kupumua, kutoa miruzi kwenye njia ya hewa, kuwashwa ngozi, kuvimba koo na kushuka kusiko kwa kawaida kwa shinikizo la damu.

 

Dawa zinazoweza kusababisha shinikizo la chini la damu

​

  • Dawa ya kuongeza kukojoa ( au kupoteza maji) mfano frusemide au Lasix, hydrochlorothiaxide

  • Dawa aina ya alpha blockers kama prazosin

  • Dawa aina ya beta blocker kama atenolol, propranolol

  • Dawa kwa matibabu ya tatizo la parkinsonism mfano pramipexole na levodopa

  • Dawa za kuzuia huzunika mfano doxepin na imipramine

  • Dawa za kutibu matatizo ya kushindwa kusimamisha uume mfano sildenafir, tadalafil

​

Aina za shinikizo la chini la damu

​

Shinikizo la damu la chini limegawanyika kulingana na visababishi na mambo mengine

​

Shinikizo la damu la chini wakati wa kusimama

​

Hutokea endapo mtu amekaa ghafla au amesimama ghafla kutoka kwenye pozi la kulala.

Kwa asili mwili  huongeza mapigo ya moyo na mishipa ya damu husinyaa ili kuongeza shinikizo la damu kwenye mishipa ili damu iweze fika kwenye ubongo.  Watu wanaopata shinikizo la chini la damu wakati wa kusimama, njia hii ya asili ya kupandisha shinikizo la damu hufeli kufanya kazi na shinikizo la damu hushuka chini na kupelekea kupata dalili zote za shinikizo la chini.


Shinikizo la damu kutokana na kubadili pozi huweza kusababishwa na mambo mablimbali ikiwa pamoja na kuishiwa maji mwilini, kulala kwa mda mrefu, ujauzito, kisukari, kuungua, joto kali, kuvimba kwa mishipa ya vena na magonjwa fulani ya mishipa ya fahamu.

​

Baadhi ya dawa zinazoweza kusabaisha shinikizo la damu la chini wakati wa kusimama ni pamoja na dawa jamii ya kupunguza maji mwilini, beta bloka, dawa vipingzmizi vya Kalisimu na dawa vizuizi vya kimen'enya angiotensin, dawa jamii ya antidiprisanti, dawa zinazotumika kutibu ugonjwa wa  Parkinson's na kushindwa kusimamisha uume.


Tatizo hili hutokea sana kwa wazee, lakini pia hudhuru vijana wadogo ambao wanasimama kwa ghafla kutoka kwenye pozi la kukaa wakiwa wamekunja nne au kuchuchumaa kwa mda mrefu.

Kwa baadhi ya wakati shinikizo la damu la chini la aina hii huweza kuchelewa kwa dakika 5 hadi 10 baada ya mtu kusimama kutoka kwenye pozi la kulala.

 

Shinikizo la damu la chini baada ya kula chakula

​

Hutokea mara tu baada ya mtu kumaliza kula chakula na hudhuru wazee. Mtu anapokula chakula damu huwa inaelekea sana tumboni na kwenye utumbo kwa kusudi la kuchukua chakula kilichomeng’enywa. Kwa kawaida mwili husinyaza baadhi ya mishipa na kuongeza mapigo ya moyo ili kuhakikisha mwili unabaki na shinikizo la damu la kawaida, bahati mbaya kwa baadhi ya watu kitendo hiki hufeli kufanyika na kusababisha shinikizo la damu la chini. Matokeo yake ni mtu kupata dalili zote za shinikizo la damu la chini

​

Shinikizo la damu la chini hudhuru mara nyingi watu wenye shinikizo la juu la dmau na wale wanaougua magonjwa ya mfumo wa fahamu mfano ugonjwa wa Parkinson's

Ili kujikinga na madhara haya, kula chakula chenye wanga kiasi na punguza dozi za dawa za kushusha presha.

​

Shinikizo la damu la chini kutokana na kufeli kwa mfumo wa fahamu wa ubongo

Hili tatizo hutokea kwa vijana wadogo wanaosimama kwa muda mrefu na husababishwa kwa kufeli kwa mawasiliano kati ya moyyo na ubongo. Mtu huanza kupata dalili za shinikizo la dmau la chini kabla ya kuanguka.

 

Shinikizo la damu la chini kwa sababu ya kuharibiwa kwa mishipa ya fahamu  inayoongoza matendo yasiyo ya hiari

Mfano mapigo ya moyo, kupumua, kubeng’enya chakula na shinikizo la damu. Uharibifu huu huweza kusababishwa na tatizo la shy-Drager syndrome

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba kabla ya kuchukua hatua yoyote ya kitiba baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kubofya 'Pata Tiba,  au ''mawasiliano yetu' chini ya tovuti hii

Imeboreshwa,

21 Novemba 2024 05:07:12

Rejea za mada hii:

Hypotension. National Heart, Lung, and Blood Institute. https://www.nhlbi.nih.gov/book/export/html/4880. Imechukuliwa 16.04.2020

Low blood pressure. American Heart Association. http://www.heart.org/HEARTORG/Conditions/HighBloodPressure/AboutHighBloodPressure/Low-Blood-Pressure_UCM_301785_Article.jsp. Imechukuliwa 16.04.2020

Kaufman H, et al. Mechanisms, causes and evaluation of orthostatic hypotension. http://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 16.04.2020

Understanding blood pressure readings. American Heart Association. http://www.heart.org/HEARTORG/Conditions/HighBloodPressure/AboutHighBloodPressure/Understanding-Blood-Pressure-Readings_UCM_301764_Article.jsp. Imechukuliwa 16.04.2020

Kaplan NM, et al. Ambulatory and home blood pressure monitoring and white coat hypertension. http://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 16.04.2020

Kaufman H, et al. Treatment of orthostatic and postprandial hypotension. http://www.uptodate.com/home. Imechukuliwa 16.04.2020

bottom of page