Vidokezo vya Afya

Homoni estrogen inahusishwa na saratani ya titi
Kuvunja ungo mapema, kuchelewa uzazi wa kwanza, kutonyonyesha, kuchelewa koma hedhi na kutumia dawa za uzazi wa mpango huanika matiti yako kwenye homoni estrogen, kihatarishi cha saratani ya titi. Jenga tabia ya kujichunguza endapo una moja ya kihatarishi.

Ili mwanao ale vema, muonyeshe mfano
Mzazi unaweza kuwa mfano mzuri wa kuigwa na mwanao katika suala la kupenda kula vyakula vya kiafya. Kuwa mfano chanya kwa kula vyakula vya kiafya kama matunda aina tano na mboga za majani kila siku huku ukiachana na vyakula au vinywaji vyenye sukari kwa wingi. Mwanao akila vyakula mbalimbali vya kiafya hatakataa chakula na atakuwa vema kimwili na kiakili.

Imarisha kinga ya mwili wako kwa chakula
Uwezo wa mwili kupambana na maradhi hutegemea kile unachokula. Kuuongezea mwili wako uwezo wa kukukinga na kuponya maradhi ya virusi, bakteria na fangasi, tumia mara kwa mara vyakula kama vile matunda yenye uchachu, pilipili hoho, tangawizi, vitunguu swaumu, spinachi n.k. Kula vema ujiepushe na maradhi.


