top of page

Maelezo ya majibu ya maswali mbalimbali ya kiafya

Kuota upele mweusi katika umee husababishwa na nini?

Vijinundu au vipele vyeusi kwenye uume mara nyingi si hatari. Kwa watu wenye ngozi nyeusi, hata vipele vya kawaida kama vipele lulu au Fordyce huonekana kahawia au vyeusi. Visababishi vingine ni sunzua (HPV), molaskamu, doa la dawa linalorudi sehemu ileile kila unapotumia dawa fulani (fixed drug eruption), madoa yaliyobaki baada ya kidonda au muwasho, na mara chache kaswende au saratani ya mwanzo. Kinundu kinachokua, kidonda kisichopona au kinachotoa damu kinahitaji uchunguzi.

Aina za mimba zisizo za kawaida ni zipi?

Mimba zisizo za kawaida hutofautishwa kwa dalili, uchunguzi wa mlango wa kizazi na ultrasound: mimba inayotishia kutoka (damu, mlango umefungwa, mimba hai – nusu huendelea); isiyoepukika (mlango umefunguka); isiyokamilika (sehemu imetoka, mabaki yamebaki); iliyokamilika (yote imetoka, damu imepungua); iliyofia tumboni bila kutoka (missed miscarriage – mara nyingi bila dalili); mimba nje ya kizazi (hatari ya kupasuka); na mimba zabibu (molar – kutapika sana, tumbo kubwa kuliko umri, hCG juu sana). Kila moja ina matibabu tofauti – kusubiri, dawa, MVA, upasuaji au ufuatiliaji wa hCG.

Plaki

Plaki ni neno la kitaalamu la mabadiliko ya ngozi: eneo lililoinuka kidogo juu ya ngozi, lenye upana mkubwa kuliko kimo chake (kwa kawaida zaidi ya sentimita 1), lenye mipaka inayoonekana. Linaweza kuwa jekundu, kahawia, zambarau au jeupe, laini au lenye magamba. Si ugonjwa wenyewe – ni dalili. Visababishi vikuu ni soriasisi, ukurutu wa muda mrefu, licheni sugu ya ngozi, fangasi, lupus ya ngozi, na kwa mwenye VVU – saratani ya Kaposi.

Ukipata homa na mafua siku ya pili baada ya tukio la hatari, inaweza kuwa maambukizi ya VVU?

Hapana, si kawaida. Dalili za mwanzo za VVU (homa, koo kuuma, vipele, mitoki kuvimba, uchovu) – kwa wale wanaozipata – huanza wiki 2 hadi 4 baada ya kuambukizwa, si siku 1 au 2. Homa na mafua siku ya pili mara nyingi ni mafua ya kawaida, influenza, COVID-19 au maambukizi mengine. Jambo muhimu zaidi baada ya tukio la hatari si dalili – ni kupata PEP ndani ya saa 72 na kupima kwa wakati sahihi.

Vyakula vinavyoongeza uzalishaji wa maziwa ya mama baaada ya kujifungua

Kiasi cha maziwa ya mama hutegemea zaidi mtoto kunyonya mara kwa mara na kwa ufanisi: kadiri maziwa yanavyotoka, ndivyo yanavyotengenezwa zaidi. Lishe bora, maji ya kutosha, kupumzika na utulivu wa akili husaidia. Vyakula kama uji, karanga, mboga za majani, viazi vitamu, karoti, tangawizi, kitunguu saumu na fenugreek hutumika kuongeza maziwa. Tafiti ndogo zimeonyesha faida kwa baadhi ya vyakula hivi, lakini tafiti kubwa zinahitajika. Ladha ya maziwa hubadilika kidogo kulingana na chakula, na hili si tatizo. Mama wengi wanaodhani maziwa ni machache kwa kweli yanatosha.

Vinywaji vya kuongeza nguvu mwilini

Vinywaji vya kuongeza nguvu (energy drinks) huwa na kafeini, sukari nyingi na viungo kama taurine. Kopo moja la ml 250 lina kafeini takriban mg 80 na sukari takriban gramu 27 (vijiko 6–7). Kwa mtu mzima, kafeini hadi mg 400 kwa siku (makopo 4–5 madogo) huonekana salama, lakini kunywa mengi kwa wakati mmoja, kuchanganya na pombe, au kwa wenye ugonjwa wa moyo, huweza kuleta moyo kwenda kasi, presha kupanda, kukosa usingizi na mara chache shambulio la moyo hata kwa vijana. Havifai kwa watoto, wajawazito na wanaonyonyesha.

bottom of page