Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
Dkt. Benjamin L, MD
Dkt. Sospeter B, MD
31 Oktoba 2026, 15:23:43

Madini chuma kwa mjamzito
Jibu kwa ufupi
Jibu kwa ufupi: Meza kidonge cha madini chuma na foliki asidi kila siku kama ulivyopewa kliniki. Kimeze na chungwa, embe au maji – si chai, kahawa wala maziwa. Kula maharage, dagaa, maini, nyama na mboga za majani. Soma Upungufu wa damu kutokana na ukosefu wa madini chuma.
Maelezo
Kwa nini ni muhimu
Hupunguza hatari ya upungufu wa damu kwa mama.
Hupunguza hatari ya mtoto kuzaliwa na uzito mdogo.
Mama mwenye damu ya kutosha hustahimili vizuri damu inayopotea wakati wa kujifungua.
Vitu vinavyoongeza ufyonzwaji
Vitamin C – machungwa, maembe, mapera, ndimu, nyanya.
Nyama, maini, samaki, dagaa – chuma chake hufyonzwa kwa urahisi na huongeza ufyonzwaji wa chuma cha mimea.
Kuloweka, kuotesha au kuchachusha nafaka na kunde (mfano togwa, uji wa kuchachuka).
Vitu vinavyopunguza (vitenganishe na dawa)
Chai na kahawa.
Maziwa, maziwa mgando, jibini na dawa za calcium.
Dawa za kupunguza asidi tumboni.
Tenganisha saa 1–2 na dawa – si kuacha vyakula hivi.
Visababishi vingine vya upungufu wa damu
Malaria – tumia chandarua na dawa za kinga (SP) unazopewa kliniki; soma Dawa nzuri ya malaria.
Minyoo – dawa ya minyoo hutolewa kliniki baada ya miezi 3 ya kwanza.
Magonjwa ya utumbo yanayopunguza ufyonzwaji, mfano kuharisha kwa muda mrefu.
Nini cha kufanya
Meza dawa kila siku – hata ukijisikia vizuri.
Kinyesi kuwa cheusi ni kawaida ukitumia madini chuma.
Kichefuchefu: meza wakati wa kulala au baada ya mlo mdogo.
Choo kigumu: kunywa maji mengi, kula matunda na mboga.
Dalili za hatari
Hospitali mara moja ukiwa na:
Kushindwa kupumua au kuchoka sana hata ukiwa umepumzika.
Mapigo ya moyo kwenda kasi sana au kuzimia.
Kutokwa damu ukeni.
Lini umwone daktari
Uchovu mkubwa, kizunguzungu, ngozi na viganja kupauka – soma Dalili za awali za upungufu wa damu.
Huwezi kuvumilia dawa kwa sababu ya kichefuchefu au kutapika.
Hujapimwa damu kliniki.
Maswali yanayoulizwa mara kwa mara
1. Kidonge cha madini chuma nimeze na nini?
Maji au tunda lenye vitamin C kama chungwa.
2. Naweza kunywa chai na dawa?
Hapana; tenganisha saa 1 hadi 2.
3. Matunda na mboga za majani hupunguza madini chuma?
Hapana; matunda yenye vitamin C huongeza ufyonzwaji.
4. Kinyesi kimekuwa cheusi, ni hatari?
Hapana, ni kawaida kwa dawa za madini chuma.
5. Damu chini ya kiasi gani ni upungufu kwa mjamzito?
Hb chini ya 11 g/dL.
6. Nikijisikia vizuri niache dawa?
Hapana; endelea kama ulivyoelekezwa kliniki.
7. Vyakula gani vina madini chuma kwa wingi?
Maini, nyama, dagaa, maharage, mboga za majani kama mchicha na matembele.
8. Malaria inapunguza damu?
Ndiyo; jikinge na tumia dawa za kinga za kliniki.
Imeandikwa:
2 Aprili 2026, 19:17:50
ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.
Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.
Rejea za mada hii:
World Health Organization. WHO recommendations on antenatal care for a positive pregnancy experience. Geneva: WHO; 2016.
World Health Organization. Guideline: daily iron and folic acid supplementation in pregnant women. Geneva: WHO; 2012.
Hurrell R, Egli I. Iron bioavailability and dietary reference values. Am J Clin Nutr. 2010;91(5):1461S–7S.
Pena-Rosas JP, De-Regil LM, Garcia-Casal MN, Dowswell T. Daily oral iron supplementation during pregnancy. Cochrane Database Syst Rev. 2015;(7):CD004736.
Pamplona-Roger GD. Encyclopedia of Foods and Their Healing Power. Vol. 1. Education and Health Library; 2004.
Ministry of Health, United Republic of Tanzania. Standard Treatment Guidelines and National Essential Medicines List (STG/NEMLIT), 7th edition. Dodoma: Ministry of Health; 2026.

