top of page
Dalili za saratani ya ulimi
Dawa za kusafisha ulimi
Dawa ya vidonda kwenye ulimi

Imeandikwa na ULY CLINIC

Kabla ya kusoma makala hii kumbuka mambo yafuatayo;

ULY CLINIC inakushauri siku zote ufuate ushauri kutoka kwa mtaalamu wa afya anayetambulika na mwenye leseni ili uepuke madhara ya kiafya yanayoweza kukupata.

 

Tafuta ushauri na tiba kutoka kwa daktari wako kila mara unapopatwa na shida kabla ya kuchukua hatua yoyote ile, naam hata baada ya kusoma makala hii, daktari wako atakufanyia uchunguzi kujua tatizo lako na kukushauri tiba kulingana na tatizo lako.

Wasiliana na daktari wa ULY Clinic kwa ushauri zaidi na tiba kupitia namba za simu chini ya tovuti hii.

Ulimi

Makala hii ni mahususi kujibu maswali mbalimbali kwa kifupi kuhusu ulimi. KWa maelezo zaidi mara baada ya kusoma bonyeza linki itakayokuunga moja kwa moja kusoma makala husika

Maswali yaliyojibiwa hapa kuhusu ulimi ni (bonyeza kichwa cha mda kuenda kwneye maelezo zaidi)

Dalili za saratani ya ulimi

 

Aina kadhaa za saratani zinaweza kuathiri ulimi na mara nyingi huanzia kwenye ukuta wa ngozi ya ulimi uliotengenezwa na seli za squamous. Matibabu na hatima ya saratani ya ulimi hutegemea aina ya saratani iliyoathiri ulimi. Saratani ya ulimi inayotokea sehemu za mdomo ambapo itakuwa rahisi kuonekana kwa macho huweza kutibiwa mapema mara inapoonekana na kuzuia madhara, saratani ya ulimi inayotokea nyuma karibu na koo au kwenye shina la ulimi si rahisi kuonekana na hivyo huweza kugunduliwa katika hatua za juu Zaidi wakati tatizo tayari limeshakuwa kubwa.

 

Dalili za saratani ya ulimi hutegemea hatua ya sawatani, baadhi yake ni;

 • Kidonda kwenye ulimi ambacho hakiponi

 • Uvimbe kwenye ulimi

 • Maumivu ya ulimi yanayoambatana na uvimbe au kidonda

 • Maumivu wakati wa kumeza chakula

 • Kumeza kwa shida

 • Mabadiliko ya sauti (kuwa na sauti kama ya farasi au sauti kukauka)

 • Maumivu kwenye taya

 • Kuhisi kitu kinakaba kwenye koo

 • Shida katika kumeza au kutafuna chakula

 • Vidonda kwenye ulimi ambavyo haviponi

 • Ganzi mdomonikutokwa na damu kwenye ulimi bila sababu

 • Uvimbe kwenye ulimi ambao hauondoki

Soma zaidi makala hii kwa kubonyea hapa

Dawa za kusafisha ulimi

 

Kusafisha ulimi kila baada ya kula kunaweza kukusaidia kuondoa uchavu pamoja na hatari ya magonjwa ya kinywa na harufu mbaya. Watu wengi wamekuwa wakisafisha ulimi kwa kutumia dawa za meno, lakini kuna dawa zingine ambazo zinaweza kutumika kusafisha kinywa chako na kukiweka katika hali nzuri ya kiafya.

Baadhi ya tafiti zinasema kwamba kusafisha ulimi kwa kutumia kifaa cha kukwangua ulimi au mswaki ni njia nzuri Zaidi ya kusafisha ulimi. Hata hivyo matumizi ya mswaki na dawa za kuosha kinywa pia husaidia mara nyingi kuweka kinywa chako safi;

Baadhi ya dawa za kusafisha ulimi ni pamoja na;

 • Unga wa baking soda- husafisha ulimi kwa kuondoa na kuua fangasi aina ya candida pamoja na bakteria streptococci

 • Chlorhexidine gluconate 

Dawa ya vidonda kwenye ulimi

Vidonda kwenye kinywa kwa jina jingine hufahamika kama vidonda vya kanka, huwa ni vidonda vidogo vinavyouma, hutokea kwenye sakafu ya fizi. Vidonda hivi husababisha usumbufu wakati wa kula na kutafuna kwani huuma sana wakati huu.

 

Dawa na mambo unayoweza kufanya  kutibu vidonda kinywani ni pamoja na;

 • Kutumia maji yenye baking soda kusukutua kinywa chako mara mbili hadi tatu kwa siku

 • Kuweka uji wa magniziamu kwenye kidonda

 • Kufunika/kupaka uji wa baking soda kwenye kidonda

 • Kutumia benzocaine (tafuta ushauri wa daktari kwanza) kupunguza maumivu

 • Kutumia barafu kwa kuilamba au kuiweka karibu na kidond kupunguza maumivu

 • Dawa jamii ya steroid kupunguza uvimbe na maumivu

 • Kutumia dawa ya mswaki

 • Matumizi ya viinirishe kama foliki acid

 • Matumizi ya vitamin B6 na 12

 • Matumizi ya madini ya zinki

 • Matumizi ya dawa asilia kama majani ya chai yam mea wa chamomile

Soma zaidi kuhusu vidonda kwenye ulimi kwa kubonyeza hapa

Maumivu ya ulimi

Maumivu ya ulimi  husababishwa na hali au magonjwa mbalimbali, maumivu hayo huwa ya aina tofauti, mfano kuhisi ulimi unawaka moto au kuchoma choma wakati wa kula au kunywa, mara unapoamka tu na kudumu  siku nzima au maumivu ya kuja na kuondoka au maumivu hayo kuwepo muda wote na pengine kudumu kwa miaka kadhaa.

Sababu zinazopelekea maumivu ya ulimi huwa ni

 • Saratani ya ulimi

 • Upungufu wa damu

 • Maambukizi ya virusi vya Herpes

Endelea kusoma makala hii kwa kubonyeza hapa

Ulimi wenye kamba

Ulimi wenye kamba kwa chini au  Ulimi kushikwa ni hali inayotambuliwa  kwa mtoto wakati wa kuzaliwa, hali hii hupelekea ulimi wa mtoto kuwa na uhuru kidogo wa miendo inayotakiwa kama binadamu wa kawaida

 

Mtoto mwenye Ulimi ulioshikwa huwa na utando ama ukuta mpana ulio chini ya ulimi na unashikamanisha ulimi kwenye sakafu ya kinywa. Mtu mwenye tatiazo la ulimu kifungoni huwa na tatizo la kutoweza kutoa ulimi nje yam domo, pia huathiri ulaji wa mtoto.

Wakati mwingine tatizo la ulimi kushikwa halisababishi tatizo llote lile, tatizo hili huhitaji matibabu ya upasuaji ili kuuweka ulimu kuwa huru.

Soma zaidi kuhusu makala hii kwa kubonyeza hapa

Magonjwa ya ulimi

 

Kuna zaidi ya magonjwa kumi ya ulimi, magonjwa hayo yanaweza kusababishwa na majeraha, maambukizi ya bakteria, fangasi au virusi pamoja na saratani. Sehemu hii imeorodhesha baadhi ya magonjwa yanayotokea sana kwenye ulimi;

 • Thrashi( fungasi kwenye ulimi)- husababishwa na maambukizi ya fangasi aina ya candida, hutokea kwa watu wenye kinga ya mwili iliyo dhaifu

 • Ulimi vinyweleo vyeusi- husababisha ulimi uonekane wenye vinyweleo vyenye rangi nyeusi bila maumivu yoyote. Tatizo hili hutokea pale endapo vinyweleo vya ulimi vimekuwa virefu na kuwavutia bakteria wa kinywa kufanya makazi na kuzaliana na kuanya ulimi uonekane mweusi wenye vinyweleo vingi. Visababishi vingine ni pamoja na matumizi ya dawa za antibayotiki, kutosafisha ulimi vema, kuvuta sigara, kunywa kahawa kwa wingi, na kutozalishwa kwa mate ya kutosha.

 • Vidonda vya kanka, hutokea sana kwenye kuta za kinywa na au kwenye ulimi, hupona ndani ya siku chache hadi wiki mbili, vidonda hivi huleta maumivu wakati wa kula au kunywa (bonyeza hapa kusoma zaidi)

 • Licheni planazi- ni harara zinazotokea kwa nadra sana, huonekana kama mwinuko wenye rangi nyeupe, miinuko hii huwa na ukubwa tofauti tofauti na huwa na sifa ya kungaa na hukaa kwenye ulimi au kwenye mashavu ya midomo. Tatizo hili huambatana na maumivu pamoja na vidonda kwenye kinywa na ulimi. Huweza kutibiwa kwa kutumia dawa za kunywa au kupaka. Endapo tatizo ni sugu huweza kupelekea kuwa saratani. Ugonjwa huu huweza kuathiri sehemu zingien za ngozi katika mwili pia.

 • Ulimi jiografia/ulimi ramani- Ulimi wa jiografia au ulimi ramani(ilimi kuwa na mabaka) kwa lugha ya kiingereza "geographic tongue" hutokana na ni michomo ya kinga za mwili ambayo huathiri sakafu ya juu au kwenye pembe za kushoto na kulia ya ulimi. Tatizo hili halina madhara yoyote kwa binadamu. Tafiti nyingi zimeonesha ulimi jiografia huambatana na matatizo ya pumu ya Ngozi, licheni planas na soriasisi (bonyeza hapa kusoma zaidi)

 • Saratani ya ulimi- Aina kadhaa za saratani zinaweza kuathiri ulimi na mara nyingi huanzia kwenye ukuta wa ngozi ya ulimi uliotengenezwa na seli za squamous. Matibabu na hatima ya saratani ya ulimi hutegemea aina ya saratani iliyoathiri ulimi. Visababishi vinaweza kuwa, uvutaji wa sigara, kunywa kupindukia(pombe) kukaa kweney jua kwa muda mrefu, historia ya saratani kwenye familia, maambukizi ya virusi vya HPV. (bonyeza hapa kusoma zaidi)

 • Vipele vya uongo- kutokana na historia, vipele hivi vinasemekana hutokea endapo mtu akisema uongo. Vipele hivi hutokana na shambulio la kinga za mwili kwenye ulimi na hutokea hata kama wewe unazungumza ukweli mtupu. Hupotea vyenyewe ndani ya siku kadhaa lakini husababisha hofu kwa mtu. Visababishi huweza kuwa ni mwitikio wa kinga za mwili dhidi ya chakula(aleji) au majeraha madogo kwenye ulimi kutokana na kujing’ata ulimi. Huhitaji matibabu lakini endapo maumivu ni makali unaweza kutumia dawa kuweka kinywani ili kupunguza maumivu. Soma hapo chini kuhusu ugonjwa wa kawasaki

 • Leukoplakia-Ulimi huonekana kuwa na rangi nyeupe kama maziwa mgando, ugonjwa huu hutokea kwa watu wenye kinga za mwili za chini kutokana na magonjwa yanayoshusha kinga za mwili, matumizi ya dawa za saratani n.k

 • Ugonjwa wa Kawasaki- huonekana kweye ulimi kwa kusababisha ulimi kuwa na rangi nyekundu sana na vipele vidogo- huu huwa dalili za awali za ugonjwa wa Kawasaki au homa ya skaleti

 • Upungufu wa vitamin B3- husababisha ulimi kuwa na rangi nyekundu lakini huwa mlaini na wenye kuuma. 

 • Ulimi kuwa mkubwa kupita kiasi(makroglosia)

 • Ulimi uliopasuka/ulimi mifereji-Ulimi uliopasuka na kuwa na mifereji (ulimi kuchanika) ni tatizo linalojulikana sana, tatizo hili hutokana na matatizo asili ya kiuumbaji na hakuna kisababishi kinachofahamika kusababisha tatizo hili. Hata hivyo tatizo hili si saratani wala halina hatari ya kuwa saratani. (bonyeza hapa kusoma zaidi)

Ulimi kuwasha

Visababishi vikuu vya ulimi kuwasha huwa ni vidonda vya kanka, kuvimba kwa tezi radha, majeraha kwenye ulimi, sindromu ya kinywa kuwaka moto, kucheua tindikali na fangasi kinywani. Baadhi ya sababu zinaweza kudhibitiwa dalili zake kwa matibabu ya nyumbani yaliyoorodheshwa hapa chini kabla au pamoja na dawa utakazoandikiwa na daktari wako. Soma zaidi kuhusu kuwasha ulimi na maumivu ya ulimi kwa kubonyeza hapa

Matibabu ya nyumbani ya ulimi kuwasha;

Matibau ya nyumbani yanatakiwa kuambatana na usafi wa kinywa. Fanya mambo yafuatayo kujitibu;

 • Acha matumizi ya vyakula vyenye pilipili au viungo kwa wingi na vyakula vinavyochokoza ulimi kama nanasi, limao na nyanya. Mbadala wake kula vyakula laini na vinavyoshauriwa kiafya

 • Tumia vidonge vya vitamin endapo unaupungufu wa vitamin haswa vitamin B3. Wasiliana na daktari wako kabla ya kutaka kutumia dawa hizi akushauri kama ni sahihi kwako

 • Matumizi ya dawa za kupunguza maumivu kwenye ulimi na kuzuia isipate uchokozi zaidi kama benzocaine na hydrogen peroxide- hakikisha unawasiliana na daktari kabla ya kutumia dawa hizi

 • Tumia vipande vya barafu kwa kuviweka mdomoni, kunywa maji ya baridi au nyonya barafu- hii itakusaidia kupunguza dalili hizi za ulimi kuwaka kuwasha na kuwaka moto.

 • Kama unatatizo la kucheua tindikali au kuzalisha tindikali kwa wingi kutoka tumboni, matumizi ya dawa za kupunguza uzalishaji wa tindikali(antacid) huweza kusaidia kupunguza na kuondoa dalili

 • Tumia majani ya chai ya chamomile. Majani haya husemekana kuwa na uwezo wa kuzuia uchokozi wa kinga za mwili au vyakula kwenye ulimi. Tumia maji yenye majani haya kwa wingi kusukutua kinywa chako wakati maji yamepoa au weka kifuko cha majani haya kwenyevidonda vilivyo kwenye ulimi.

 • Matumizi ya mafuta ya nani- mafuta haya huwa na uwezo wa kuponya vidonda vya ulimi kwa sababu huwa na kemikali za kuua fangasi na bakteria na baadhi ya virusi. Paka mafuta kwenye vidonda kwa kutumia pamba na kisha sugua taratibu au unaweza kuyaweka kinywani kwa muda kiasi kisha utatema baadaya dakika 3 hadi 5

 • Matumizi ya maji yenye chumvi kusukutulia kinywa huweza kupunguza maumivu ya ulimi na miwasho pamoja na kupunguza hatari ya maambukizi kwenye kinywa. Weka chumvi kijiko kimoja cha chai kwenye kikombe cha chai chenye maji ya uvuguvugu kisha tia kinywani na sukutua na kuyaacha kwa muda wa dakia2 kisha yateme

 • Matumizi ya asali husaidia kuponya pia vidonda, asali huwa na kemikali ambazo hufanya kazi za kupambana  na baadhi ya maambukizi ya bakteria. Paka asali moja kwa moja kwenye ulimi au kwenye kidonda kilicho kwenye ulimi kwa muda wa siku kadhaa mpaka utakapopona

 • Matumizi ya magadi soda- kwa ajili ya kutibu maumivu na kuvimba, safisha kinywa chako kwa kutumia maji ya uvuguvugu yenye magadi soda kijiko kimoja cha chai kwa nusu kikombe cha chai. Unaweza pia kupaka magadi soda moja kwa moja kwenye ulimi au kwenye kidonda.

 • Kutumia uji wa magniziamu kupaka kwenye ulimi au kidonda husaidia pia kupunguza maumivu ya ulimi na miwasho kutokana na kuungua kwa tindikali.

 • Matumizi ya maji ya hydrogen peroxide-hutibu mambukizi na vidonda ndani ya kinywa na ulimi. Tumia mchanganyiko wenye asilimia 3 ya hydrogen peroxide na changanya na maji kuepuka kuungua. Chovya pamba katika maji haya kisha gandamiza pamba hiyo kwenye kidonda kwa sekunde chache na kisha sukutua kinywa chako kwa maji ya uvuguvugu na kutema.

 • Maji ya alovera- huweza kutumika kutibu magonjwa ya kinywa, sukutua kinywa chako kwa sekunde 30 kisha tema, fanya hivi mara mbili au tatu kwa siku moaka utakapopona

Kujing’ata ulimi

 

Kujing’ata ulimi ni jambo ambalo si geni, hutokea karibia kwa watu wengi na huwa ni kwa bahati mbaya. Unaweza kung’ata ulimi wako wakati unakula, baada ya kuchonywa dawa za ganzi kwenye meno, wakati umelala, wakati una msongo wa mawazo, ukipigwe nadegedege au wakatu unashiriki mazoezi au michezo ya moira n.k

Watu wengi hupata majeraha kidogo wanapojing’ata ulimi kiasi kwamba hawahitaji kuonana na daktari isipokuwa endapo wanatokwa  damu kwa wingi bila kukauka. Vidonda vidogo vinavyotokanana kung’ata ulimi hupona ndani ya siku chahce mpaka wiki au mwezi, vdonda vikubwa huwa haviponi haraka na vinahitaji matibabu kutoka kwa daktari wako na wakati mwingi huhitaji kushonwa ili kusaidia vipone kwa haraka. Vidonda vikubwa vinaweza kuchukua wiki kadhaa hadi miezi kadhaa kupona.

Dalili zifuatazo zikupe hofu ya kutafuta matibabu ya haraka mara baada ya kujing’ata ulimi

 • Endapo unatokwa na damu nyingi sana

 • Kutokwa na damu upya marabaada ya damu kukatika

 • Kidonda kuonekana kimevimba au chenye rangi nyekundu

 • Kuhisi joto kwenye kidonda cha ulimi

 • Kutokwa na majimaji mekundu au usaha kwenye kidonda

 • Kidonda kikiwa kinauma sana

 • Kama unapata homa

 • Kuharibika kwa umbile la ulimi

 

Matibabu ya nyumbani

 

Fanya mambo yafuatayo kwa matibabu ya nyumbani;

 • Hatua ya kwanza- Nawa mikono yako kwa maji yenye sabuni kisha vaa glavu

 • Hatua ya pili- Sukutua kinywa chako kwa maji safi ili uweze kuona kidonda kilipo vema

 • Hatua ya tatu- Gadamiza kidonda kwa kutumia gozi au kitambaa kisafi kwenye eneo lilalotoka damu kwa muda wa dakika 5 ili kuzuia damu kutoka

 • Funga vipande vidogo vya barafu kwenye kitambaa kisha gandamizia kwenye eneo lenye kidonda endapo lina uvimbe

 • Mpigie daktari wako endapo damu zinaendelea kutoka hata mara baada ya kurudia hatua ya tatu iliyoorodheshwa hapo juu au endapo jeraha ni kubwa na damu zinatoka nyingi.

 

Mambo mengine unayotakiwa kufahamu na kuyafanya;

 

 • Kula vyakula laini na vyepesi kumeza

 • Tumia dawa za kupunguza maumivu kama parasetamo au ibrupofeni ili kupunguza maumivu na uvimbe

 • Tumia barafu kukanda eneo lililovimba kwa dakika 5 kwa siku

 • Sukutua kinywa chako kwamaji yenye chumvi. Changanya chumvi Kijiko kimoja cha chai kwa kikombe kimoja cha chai chenye maji ya uvuguvugu

Soma zaidi kwa kubonyeza kung'ata ulimi usingizini, au tatizo la kujing'ata ulimi kwa ujumla

Imeboreshwa mara ya nwisho, 10.11.2020

Vidonda kwenye ulimi
Maumivu ya ulimi
Ulimi kushikwa
Magonjwa ya ulimi
Ulimi uliopasuka pasuka
Ulimi weny mabaka
Vipele kweney ulimi
Ulimi kuwasha
Kung'ata ulimi
bottom of page