Mwandishi:
Mhariri:
Imeboreshwa:
ULY CLINIC
Dkt. Helen L, M.D
24 Agosti 2026, 03:43:15

Usugu wa vimelea vya maradhi kwenye dawa
Matumizi yasiyo sahihi ya dawa jamii ya ‘antibiotic’ na ‘antifungal’ zinazotibu magonjwa mbalimbali kama kisonono, TB, UTI, tonses, nimonia, homa ya matumbo, fangasi ukeni n.k, husababisha vimelea kuwa sugu na kutotibika na dawa hizo. Tumia dawa kama ulivyoandikiwa na daktari wako.
Hali ya usugu wa vimelea vya maradhi kwenye dawa
Tafiti nyingi zimefanyika kuangalia ukubwa wa tatizo la usugu wa vimelea vya maradhi kwenye dawa. Tafiti hizo zinaonyesha kuwepo na ongezeko kubwa la usugu wa vimelea vya maradhi kwenye dawa za kutibu maambukizi ya bakteria na fangasi. Tatizo hili linaweza kudhuru watu wa umri wowote na taifa lolote lile na huongeza gharama kwa wagonjwa na kukaa hospitali kwa muda mrefu.
Sababu za vimelea kuwa sugu
Sababu kuu zinazochangia kutokea kwa tatizo hili ni;
Kutokuwepo kwa mwongozo wa matumizi ya dawa kwa wataalamu wa afya inayofanya mtaalamu kujichagulia dawa bila kujali ni daraja gani la dawa lianze kutumika kwanza kabla ya kwenda daraja kubwa zaidi
Matumizi ya dawa bila kuandikiwa na daktari mwenye leseni na weledi wa dawa hizo
Matumizi ya dawa bila kufanyiwa vipimo kuonyesha ugonjwa uliopo
Kuandikiwa dawa na mtu ambaye si mtaalamu wa afya
Kutumia dawa bila kukamilisha dozi nzima uliyoandikiwa na mtaalamu wa afya
Nini ufanye ili kuepuka usugu wa vimelea kwenye dawa?
Tumia dawa endapo tu umeandikiwa na daktari aliyesajiliwa
Usinunue au kutumia dawa za 'antibiotic' au 'antifungal' endapo mtaalamu amekwambia huhitaji tumia dawa hizo
Usitumie mabaki ya dawa za 'antibiotic' au 'antifungal' au kutumia kwa pamoja dozi ya mtu mwingine
Tumia dozi ya dawa kwa masaa na siku ulizopangiwa na mtaalamu wa afya
Jikinge na maradhi mbalimbali kwa kufuata kanuni za kiafya mfano, Kunywa maji safi na salama, nawa mikono kabla ya kula, andaa chakula kwa usafi, fanya ngono salama na pata chanjo kwa wakati ili uepuke matumizi ya dawa
Usitumie mazao ya wanyama au ndege waliokuzwa kwa dawa za 'antibiotic' au kutumia dawa hizo kama kinga ya maradhi ya magonjwa, isipokuwa endapo walikuwa wanaumwa. Hii itasaidia kuepuka kupata vimelea sugu kutoka kwa mazao hayo
Penda kujisomea kuhusu mada za kiafya ili kufahamu matibabu ya nyumbani, dawa, magonjwa na kinga mbalimbali za maradhi
Kumbuka;
Matumizi ya dawa yasiyo sahihi hujumuisha matumizi kwa binadamu au wanyama wengine wa kufungwa
Unaweza kupata maambukizi ya vimelea sugu wa dawa aina fulani kutoka kwa mtu mwingine au mnyama, kisha ukashindwa kutibika kwa dawa inayofahamika kutibu vimelea au ugonjwa ulionao.
Imeandikwa:
2 Aprili 2026, 19:17:50
ULY CLINIC inashauri usitegemee au kufuata ushauri wowote uliyoona kwenye makala hii bila kuwasiliana kwanza na daktari wako. Kabla ya kuchukua hatua yoyote ya matibabu, hakikisha umepata ushauri rasmi kutoka kwa daktari wako ili kuepuka madhara yoyote yanayoweza kutokea.
Makala hii ni ya kielimu tu na haitumiki kama mbadala wa matibabu ya daktari.
Rejea za mada hii:

