Mwandishi:
Mhariri:
ULY CLINIC
Dkt. Benjamin Lugonda, MD
28 Septemba 2025, 00:58:18

Rangi ya ute ukeni na maana yake kiafya
Majimaji (ute) ya kawaida yanayotoka ukeni huzalishwa na tezi ndogo zinazopatikana kwenye tundu la uke na shingo ya kizazi.
Majimaji au ute huu hutoka kila siku ili kuondoa chembe zilizokufa na uchafu na kufanya uke uwe kwenye hali safi ya kiafya. Kiasi na rangi ya majimaji yatokayo ukeni hutofautiana kila siku na kwa kila mtu mmoja na mwingine. Kiasi na rangi ya majimaji yatokayo ukeni hutofautiana kila siku na kwa kila mtu mmoja na mwingine.
Makala hii imeelezea aina za ute na maana yake kiafya. Ute umetumika kumaanisha majimaji ya kawaida au uchafu unaoweza kutoka ukeni.
Je ni rangi gani za ute unaoweza kutoka ukeni?
Kuna rangi mbalimbali za ute unaoweza kutoka ukeni, rangi hizo ni;
Ute mweupe kama maziwa
Ute wa rangi ya maji
Ute wa rangi nyekundu
Ute wa rangi ya kijivu
Ute wa rangi ya kijani
Ute wa rangi ya njano
Ute wa rangi ya bluu
Kila rangi imeelezewa hapa chini ni nini kinaweza kuwa kisababishi
Ute mweupe rangi ya maji ukeni
Ute wa kawaida ukeni huwa na rangi kama ya maji kwa watu wengine huita uta mweupe lakini weupe si kama wa maziwa bali weupe wa maji. Licha ya kuwa mweupe kama maji, pia huwa na utelezi mithiri ya uterezi wa maji ya bamia au yai .
Ute ute huzidi kuteleza zaidi na kuwa mweupe zaidi kipindi cha hatari(kipindi yai linatolewa), wakati wa kusisimuliwa kingono na wakati wa ujauzito.
Ute wa rangi ya maziwa ukeni
Kutokwa na ute wa rangi nyeupe kama maziwa ukeni ni nini kisababishi?
Kutokwa ute wa rangi ya maziwa inamaanisha kutokwa na uchafu ulio mzito na mweupe kama maziwa au kuwa laini kama mafuta mgando(krimu).
Endapo ute huo hauambatani na dalili zingine ukeni, hii humaanisha ute wa kawaida kwa ajili ya kulainisha uke.
Endapo ute huu una harufu kali huweza kuashiria maabukizi ukeni na mara nyingi humaanisha maambukizi ya ‘fangasi ukeni’ ambapo huweza kupelekea dalili zingine za muwasho ukeni.
Ute wa rangi ya njano ukeni
Kutokwa na ute wenye rangi ya njano mpauko bila kuwa na dalili zingine humaanisha ute wa kawaida kwa ajili ya kulainisha uke na huweza kusababishwa pia mabadiliko ya chakula au matumizi ya virutubisho nyongeza.
Endapo ute una rangi ya njano iliyokolea au njano inayoelekea kijani, mara nyingi humaanisha maambukizi ya 'magonjwa ya zinaa'. Dalili zingine zinazoweza kuambatana ni, harufu mbaya, kama ya kuoza samaki, majimaji kuwa mazito zaidi au mabonge.
Ute wa rangi nyekundu ukeni
Ute wa rangi nyekundu huweza kuwa na wekundu mpauko au mkoleo ama rangi ya kutu. Mara nyingi ute wa rangi nyekundu husababisha na hedhi.
Endapo ute unatoka ndani ya siku za hedhi kila mwisho wa mwezi yaani kila baada ya siku 28 hadi 35 kutoka mzunguko mmoja hadi mwingine hii humaanisha ute wa kawaida baada au kabla ya hedhi.
Endao ute wa rangi hii unatoka katikati ya mzunguko wa hedhi, hii mara nyingi huashiria matatizo mbalimbali kama matatizo ya homoni, saratani ya shingo ya kizazi n.k
Endapo ute mwekundu unaambatana na harufu kali ukeni na katikati ya hedhi au kwenye hedhi, maranyingi ina maanisha dalili za awali za saratani ya shingo ya kizazi.
Endapo upo kwenye koma hedhi kipindi angalau mwaka mmoja mfululizo na unatokwa na majimaji ya rangi nyekundu ukeni, inaweza kumaanisha saratani ya mji wa uzazi, au saratani ya shingo ya kizazi.
Ute wa rangi ya pinki ukeni
Ute wa pinki unaweza kuwa pinki mpauko au ile iliyokolea, hii husababishwa mara nyingi na uwepo wa damu kidogo.
Kutokwa na ute wa rangi ya pinki humaanisha unakaribia kuingia hedhi na endapo umeshika ujauzito, humaanisha upo kipindi cha upandikizaji wa yai lililochochavushwa mwanzoni kabisa mwa ujauzito.
Baadhi ya wanawake wakiwa siku za hatari (yai linapotolewa), hupata matone ya damu kidogo yanayoweza kupelekea ute ukeni kuwa na rangi ya pinki ambayo ni kawaida.
Ute wa pinki pia unaweza kutokea baada ya kushiriki ngono na umepata majeraha kidogo kwenye uke yaliyosababisha damu kuvia na hivyo ikachanganyika na kusababisha majimaji kuwa na rangi hiyo ya pinki.
Ute wa rangi ya kijivu ukeni
Kutokwa na ute wa rangi ya kijivu si kawaida na huweza maanisha mara nyingi maambukizi ya bakteria ukeni haswa ugonjwa wa vajinosis ya bakteria. Dalili zinazoambatana na ute au uchafu huu wa rangi ya kijivu ukeni na kumaanisha maambukizi ya bakteria ni miwasho, michomo, harufu kali kuwa na wekundu maeneo yanayozunguka mashavu na tundu la uke.
Ute wa rangi ya kijani ukeni
Kutokwa na ute wa rangi ya kijani au njano kijani ukeni mara nyingi huashiria maambukizi ya 'magonjwa ya zinaa'. Dalili zingine zinazoweza kuambatana ni harufu mbaya au kama samaki aliyeoza, ute kuwa mazito zaidi au kama mabonge.
Wakati gani unapaswa kuwasiliana na daktari haraka?
Endapo unatokwa na uchafu(ute) ukeni unaoambatana na dalili zifuatazo tafuta msaada wa daktari.
Kujihisi hali isiyo kawaida ukeni
Kutokwa na damu wakati wa kushiriki ngono
Kutokwa na damu katikati ya vipindi vya hedhi
Kutokwa na damuu baada ya komahedhi
Kutokwa na harufu mbaya ukeni kama ya kitu kilichooza (samaki)
Kutokwa na ute wa rangi ya kijani, njano au kijivu
Kutokwa na ute wenye povu
Maumivu
Muwasho wa uke
Uchafu ukeni unaoambatana na hisia za kuungua wakati wa kukojo
Wapi utapata taarifa zingine zaidi?
Soma zaidikuhusu
Soma kuhusu harufu mbaya ukeni na visababishi vyake
Soma pia kuhusu uchafu wa rangi ya bluu kijani ukeni
Kusoma kuhsu vajinosis ya bakteria
Maswali yaliyoulizwa mara kwa mara
1 Je, ni kawaida kutoka na ute kila siku?
Ndiyo, ni kawaida mwanamke kuwa na ute kila siku kwa kiwango tofauti, mradi hauna harufu mbaya, muwasho, au maumivu.
2 Ute hubadilika kulingana na siku za mzunguko wa hedhi?
Ndiyo, ute huwa mwingi na mtelezi zaidi kipindi cha ovulation (siku za hatari), na huwa kidogo au mzito zaidi siku nyingine.
3 Habari, nilikutana na mwenza wangu siku ya Jumamosi, lakini siku iliyofuata nilianza kutoka na ute mweupe mwepesi na tumbo linauma kama niko kwenye period. Je, hii inaweza kumaanisha nimepata ujauzito au nina tatizo jingine?
1. Kuhusu ujauzito
Ujauzito hauwezi kugundulika mara moja baada ya tendo la ndoa.Yai linachukua siku 6–12 hivi kujipandikiza kwenye ukuta wa mfuko wa uzazi, ndipo homoni za mimba zinaanza kutengenezwa na zinaweza kuonekana kwa vipimo.
Kwa hiyo, dalili ulizopata siku moja baada ya tendo (ute mweupe na maumivu ya tumbo) si dalili za mimba.
2. Sababu zinazowezekana za dalili zako
Ute mweupe mwepesi: Unaweza kuwa sehemu ya mzunguko wa kawaida wa hedhi (ovulation discharge) au ishara ya mabadiliko ya homoni.
Maumivu ya tumbo kama ya period: Hii inaweza kuwa dalili za kabla ya hedhi, ovulation, au wakati mwingine ishara ya maambukizi madogo ya uke au kizazi.
Ikiwa ute ungekuwa na harufu mbaya, rangi ya kijani/kahawia, ukatoa muwasho au maumivu makali, basi ingeashiria zaidi maambukizi.
3. Nini cha kufanya
Subiri hadi kipindi chako cha hedhi kiishe au uchelewe ndipo unaweza kufanya kipimo cha ujauzito cha mkojo, mara nyingi kuanzia siku ya 7 baada ya hedhi kuchelewa.
Kama dalili zitaendelea (maumivu ya tumbo, ute usio wa kawaida, muwasho, au harufu mbaya), tafadhali muone daktari au nesi wa afya ya uzazi kwa uchunguzi wa maambukizi.
Hitimisho
Dalili ulizopata siku moja baada ya tendo la ndoa hazimaanishi mimba. Zinaweza kuwa mabadiliko ya kawaida ya homoni au dalili za tatizo jingine dogo.
4 Ute wa kawaida na ule wa maambukizi unatofautishwaje?
Ute wa kawaida huwa hauna harufu mbaya, hauna muwasho, na mara nyingi hubadilika kulingana na mzunguko wa hedhi. Ute wa maambukizi mara nyingi hubadilika rangi (njano, kijani, kijivu), huambatana na harufu mbaya na muwasho.
5 Je, chakula ninachokula kinaweza kubadilisha ute wa ukeni?
Ndiyo, lishe na matumizi ya virutubisho (supplements) yanaweza kubadilisha kiasi au rangi ya ute kwa muda mfupi.
6 Kwanini wakati wa ujauzito ute huongezeka?
Kiwango cha homoni hubadilika na kuongeza uzalishaji wa ute ili kulinda kizazi na kusaidia mazingira ya mtoto tumboni.
7 Je, matumizi ya dawa za homoni au uzazi wa mpango yanaweza kuathiri ute?
Ndiyo, dawa za uzazi wa mpango au homoni nyingine huweza kupunguza au kuongeza ute kulingana na aina ya dawa.
8 Ute mweupe mzito kama maziwa bila harufu mbaya ni kawaida?
Ndiyo, mara nyingi ni ute wa kawaida wa kulainisha uke. Lakini kama unaambatana na harufu kali na muwasho, unaweza kuashiria fangasi.
9 Kwa nini ute unaweza kuongezeka baada ya kushiriki ngono?
Baada ya tendo la ndoa, ute unaweza kuongezeka kwa sababu ya msisimko wa kingono au kutokana na mbegu za kiume kuchanganyika na ute wa uke.
Ni wakati gani nitaweza kupima ujauzito ili kujua kwa uhakika?
Kawaida kipimo cha mkojo cha ujauzito hufanyika kuanzia siku ya 7 baada ya hedhi kuchelewa, na ndio kinatoa majibu sahihi zaidi.
ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.
Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii
Imeandikwa:
17 Juni 2021, 11:47:37
Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini
[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]
Rejea za mada
1. 5 Types of vaginal discharge & what they mean.
https://www.unitypoint.org/livewell/article.aspx?id=06f8f035-9f6e-4a79-bb58-9045b9d7d0d8. Imechukuliwa 16.06.2021
2. Merck manual. Vaginal discharge. https://www.merckmanuals.com/home/women-s-health-issues/symptoms-of-gynecologic-disorders/vaginal-discharge. Imechukuliwa 16.06.2021
3. Vaginal discharge. http://www.pamf.org/teen/health/femalehealth/discharge.html. Imechukuliwa 16.06.2021
4. Vaginal discharge. https://familydoctor.org/condition/vaginal-discharge/. Imechukuliwa 16.06.2021. Imechukuliwa 16.06.2021
5. Vaginal discharge. https://www.hhs.gov/opa/reproductive-health/fact-sheets/vaginal-discharge/index.html. Imechukuliwa 16.06.2021
6. Vaginal discharge. https://www.sutterhealth.org/health/teens/female/vaginal-discharge. Imechukuliwa 16.06.2021
7. Vaginal discharge.https://www.drugs.com/health-guide/vaginal-discharge.html. Imechukuliwa 16.06.2021
8. What's the cervical mucus method of FAMs?. https://www.plannedparenthood.org/learn/birth-control/fertility-awareness/whats-cervical-mucus-method-fams. Imechukuliwa 16.06.2021
