top of page

Mwandishi:

Mhariri:

Imeboreshwa:

ULY CLINIC

Dkt. Adolf S, M.D

30 Oktoba 2026, 12:50:56

shahawa-zenye-damu-ulyclinic-compressor.
Maumivu ya kifua, kifua kubana au kuwa kizito

Maumivu ya kifua, kifua kubana au kuwa kizito

Maelezo ya jumla


Maumivu ya kifua ni kati ya dalili zinazotisha zaidi kwa sababu watu huwaza moyo mara moja. Ukweli ni kwamba visababishi vingi ni vya misuli, mbavu, tindikali au wasiwasi. Lakini kwa sababu baadhi ni hatari kwa maisha – shambulio la moyo, bonge la damu kwenye mapafu, mapafu kutoboka, mshipa mkuu wa damu kuchanika – maumivu mapya ya kifua yasipuuzwe.


Makala hii ni mwongozo wa jumla. Kwa aina maalum soma Kichomi cha kifua, Maumivu ya kifua yanayoanzia shingoni na Maumivu ya tumbo na kifua wakati wa mazoezi.


Aina na jinsi inavyojitokeza


  • Kubana, uzito au kama kitu kizito kimekalia kifua, katikati, yakienea mkono wa kushoto, shingo, taya au mgongo – moyo kukosa damu (angina au shambulio la moyo).

  • Kuchoma kunakozidi ukivuta pumzi au kukohoa – utando wa mapafu: nimonia, bonge la damu, mapafu kutoboka.

  • Kuungua katikati, kupanda kooni, baada ya kula au ukilala – tindikali; soma Maumivu ya chembe ya moyo.

  • Kuuma ukibonyeza mahali pamoja, ukigeuka au kunyanyua mkono – misuli au mbavu.

  • Kuchoma kwa sekunde chache tu – mara nyingi si hatari; soma Kichomi cha kifua.

  • Kifua kubana pamoja na hofu, kupumua haraka, mikono kufa ganzi – wasiwasi.

  • Maumivu ya kuungua upande mmoja yakifuatiwa na vipele – mkanda wa jeshi.


Visababishi


Moyo na mishipa


  • Angina na shambulio la moyo – mishipa ya moyo kuziba; soma Mishipa ya ateri kuwa migumu.

  • Utando wa moyo kuvimba (pericarditis) – maumivu hupungua ukiinama mbele.

  • Mshipa mkuu wa damu (aota) kuchanika – maumivu makali sana ya kukata yanayoenda mgongoni.

  • Moyo kushindwa kufanya kazi.


Mapafu



Mfumo wa chakula



Misuli, mifupa na neva



Mengineyo



Dalili zinazoambatana


  • Kushindwa kupumua – moyo, mapafu, bonge la damu; soma Kupumua kwa shida.

  • Jasho jingi, kichefuchefu – moyo.

  • Homa na kikohozi chenye makohozi – nimonia.

  • Kukohoa damu – bonge la damu, TB.

  • Mguu mmoja kuvimba na kuuma – bonge la damu.

  • Mapigo ya moyo kwenda kasi au kuruka.

  • Kiungulia na ladha chungu – tindikali.

  • Vipele vya malengelenge upande mmoja – mkanda wa jeshi.


Dalili za hatari


Piga simu ya dharura au nenda hospitali mara moja ukiwa na:


  • Maumivu ya kubana, uzito au kuungua katikati ya kifua yanayodumu zaidi ya dakika 10 hadi 15, au yanayokuja na kurudi kila ukifanya kazi kidogo.

  • Maumivu yanayoenea mkono (hasa wa kushoto), shingo, taya, mgongo au tumbo la juu.

  • Maumivu pamoja na jasho jingi, kichefuchefu, kushindwa kupumua, kizunguzungu au kuzimia.

  • Maumivu ya ghafla ya kuchoma pamoja na kushindwa kupumua – hasa baada ya safari ndefu, upasuaji, kujifungua au mguu kuvimba.

  • Maumivu makali sana ya ghafla ya kukata yanayoenda mgongoni.

  • Kukohoa damu.

  • Mapigo ya moyo kwenda kasi sana au kuzimia.


Wakati unasubiri msaada: acha kila shughuli, kaa ukiwa umeegemea, legeza nguo, na kama huna mzio wa aspirin na umeshauriwa nayo hapo awali, tafuna kidonge kimoja cha aspirin ya kawaida. Usiendeshe gari mwenyewe.


Vipimo


  • ECG – kipimo cha kwanza kwa maumivu yoyote ya kifua yenye shaka ya moyo; hurudiwa.

  • Troponin – kipimo cha damu cha uharibifu wa misuli ya moyo.

  • X-ray ya kifua – nimonia, pafu kutoboka, maji, ukubwa wa moyo.

  • Oksijeni kwenye damu (pulse oximeter).

  • D-dimer, CT ya mapafu – shaka ya bonge la damu.

  • Echo ya moyo.

  • Kipimo cha makohozi – TB.

  • Endoskopia – maumivu ya umio na tumbo baada ya moyo kuondolewa.


Matibabu na huduma ya nyumbani


Kwa mujibu wa STG 2026, kwanza visababishi vya hatari hutambuliwa haraka – hata kama mapigo ya moyo na shinikizo la damu ni ya kawaida:


  • Moyo kukosa damu – oksijeni kama inahitajika, aspirin na dawa nyingine za kuzuia damu kuganda, dawa za maumivu, na rufaa kwa kituo chenye huduma za moyo.

  • Bonge la damu kwenye mapafu – dawa za kuyeyusha au kuzuia damu kuganda.

  • Nimonia – antibiotiki; pafu kutoboka – kutoa hewa kwa mrija.

  • Tindikali – dawa za kupunguza tindikali na mabadiliko ya ulaji.

  • Misuli na mbavu – kupumzika, joto, dawa za maumivu.

  • Wasiwasi – mbinu za kupumua, ushauri, matibabu ya muda mrefu.


Kinga


  • Acha sigara.

  • Dhibiti shinikizo la damu, sukari na lehemu.

  • Fanya mazoezi mara kwa mara na dumisha uzito unaofaa.

  • Kula mlo wenye mboga, matunda na chumvi kidogo.

  • Tembea na nyoosha miguu kwenye safari ndefu.

  • Pata chanjo ya mafua, nimonia na COVID-19 kama unastahili.


Lini umwone daktari


  • Maumivu madogo ya kifua yanayojirudia, hata kama yanaisha yenyewe.

  • Maumivu yanayokuja ukipanda ngazi au kutembea haraka na kupoa ukipumzika – angina.

  • Maumivu pamoja na kiungulia cha kila siku.

  • Maumivu ya misuli yasiyopona baada ya wiki 2.


Maswali yanayoulizwa mara kwa mara


1. Maumivu ya kifua husababishwa na nini?

Na mambo mengi: misuli na mbavu, tindikali, wasiwasi, nimonia, pumu, na moyo. Mahali, aina ya maumivu na dalili zinazoambatana husaidia kujua chanzo. Maumivu ya kubana yenye jasho au kushindwa kupumua ni dharura.

2. Kifua kinabana kama kitu kizito kimekaa juu yake, ni moyo?

Inaweza kuwa. Hisia ya uzito au kubana katikati ya kifua, hasa ikienea mkono, shingo au taya, au ukiwa na jasho, ni dalili ya moyo kukosa damu. Nenda hospitali mara moja.

3. Mapigo ya moyo kwenda kasi na kifua kuuma, dawa ni nini?

Usimeze dawa bila kujua chanzo. Hali hii inahitaji ECG kuona mapigo ya moyo. Kama kuna kizunguzungu, kuzimia au maumivu makali, nenda hospitali mara moja.

4. Nikipumua kifua kinauma na hata nikiinama, na bega pia linauma, ni nini?

Maumivu yanayozidi ukipumua yanaweza kutoka utando wa mapafu (nimonia, bonge la damu) au misuli na mbavu. Kama una homa, kikohozi au kushindwa kupumua, onana na daktari mapema.

5. Napata maumivu kifuani hadi mgongoni, ni nini?

Yanaweza kutoka misuli, umio, nyongo, kongosho au moyo. Maumivu makali sana ya ghafla yanayokata hadi mgongoni ni dharura ya mshipa mkuu wa damu. Nenda hospitali.

6. Kifua kinauma nikila chakula, ni moyo au tumbo?

Maumivu ya kuungua yanayohusiana na kula mara nyingi ni tindikali. Lakini kama yanakuja pia ukifanya kazi au ni ya kubana, chunguza moyo kwanza.

7. Je, kifua kuuma ni dalili ya UKIMWI?

Kifua kuuma si dalili mahususi ya VVU. Hata hivyo, wenye VVU wasiotibiwa hupata nimonia na TB kwa urahisi zaidi. Kama una wasiwasi, pima VVU na chunguza chanzo cha maumivu.

8. Kifua kinabana nikiwa na hofu na napumua haraka, ni moyo?

Mara nyingi ni wasiwasi au mshtuko wa hofu, hasa kwa vijana bila vihatarishi vya moyo. Lakini mara ya kwanza ifanyiwe uchunguzi ili moyo uondolewe. Soma Dalili za msongo wa mawazo.

9. Naumwa kifua na kichwa, shida ni nini?

Pamoja na homa, mara nyingi ni maambukizi kama mafua, malaria au nimonia. Bila homa, wasiwasi au shinikizo la juu la damu. Pima shinikizo la damu na onana na daktari kama inaendelea.

10. Maumivu ya kifua yameisha yenyewe, nisiende hospitali?

Kama yalikuwa ya kubana au uzito, au yalikuja ukifanya kazi, nenda hata kama yameisha – angina inaweza kutangulia shambulio la moyo. Kichomi cha sekunde chache tu mara nyingi si hatari.

ULY CLINIC inakushauri siku zote uwasiliane na daktari wako kwa ushauri na tiba zaidi kabla ya kuchukua hatua yoyote ile ya kiafya baada ya kusoma makala hii.

Wasiliana na daktari wa ulyclinic kwa ushauri zaidi na tiba kwa kutumia namba za simu au kubonyeza link ya Pata Tiba chini ya tovuti hii

Imeandikwa:

30 Oktoba 2026, 12:50:17

Soma dalili zingine Zaidi kwa kubonyeza herufi ya mwanzo hapa chini

​

[A] [B] [C] [D] [E] [F] [G] [H] [I] [J] [K] [L] [M] [N] [O] [P] [Q] [R] [S] [T] [U] [V] [W] [X] [Y] [Z] [Z] [#]

Rejea za mada hii:

  1. Ministry of Health, United Republic of Tanzania. Standard Treatment Guidelines and National Essential Medicines List (STG/NEMLIT), 7th edition. Dodoma: Ministry of Health; 2026.

  2. Recent-onset chest pain of suspected cardiac origin: assessment and diagnosis. NICE CG95; 2010 (updated 2016).

  3. Merck Manual Consumer Version. Chest pain. Merck & Co.; 2024.

bottom of page